Search This Blog

Thursday, 24 November 2016

KINYONGA NA TAUSI (sehemu ya 1)

Note: In the loving memory of my aunt, my mentor, my beloved mama 2; Naima Said Baghozi whose dream was to see her books being read by children all over the world. She may have died before publishing all her stories and seeing her dream come true, but that doesn’t mean we can’t work together to make it real. My humble request is; please subscribe to this site or bookmark this page, read the stories to your young ones and share the stories too! Thank you in advance! May Allah rest her soul in eternal peace and accept this as sadaqatul jariya from her. Ameen!




Mwandishi: Naima Baghozi

Tausi alikuwa anazunguka zunguka katika bustani kwa maringo, akitembea na mwendo wa aste aste, akiuchanua mkia wake kama ua kubwa. Kwa hakika yeye ni ndege mrembo sana na hasa pale anapochanua mkia wake. Wakati wote huo alipokuwa akiringa ringa, hakujuwa kuwa alikuwa anafuatwa na macho asiyoyaona. Anapokwenda au anapozunguka, macho yale yalikuwa yakiuandama kwa matamanio makubwa. Macho yenyewe makubwa ya kiasi kwa hivyo yalikuwa hayapitwi na jambo lolote. Mwenye macho mashuhuri hayo alikuwa ni kinyonga. Kinyonga wakati huo alikuwa na rangi moja tu ya rangi ya kunde. Lakini kinyonga hakuridhika na rangi yake basi alibaki kummezea mate Tausi kwa uzuri wake alompa Mola. Alikuwa akitamani sana kama na yeye angeweza kuwa na rangi nzuri nzuri kwenye mwili wake ili avutie kama tausi.

Kila uchao yeye alikuwa akikaa juu ya ukuta kimya na kumtazama tausi anavyojishaua na huku akili yake ikimuenda kama saa kwa mawazo. Alikuwa akipanga na kupangua vipi na yeye ataweza kuwa mrembo kama tausi. Mwisho akaamua bora amwulize tausi mwenyewe. Akamwita kwa sauti ya unyenyekevu,
“Tausi…”
“Naam kinyonga, unasemaje?”
“Mimi kila siku sina kazi ya kufanya ila kukaa hapa kwenye ukuta na kukuangalia unavyotembea kwa maringo huku na huku, hasa ukichanua mkia wako,” Kinyonga akasema.
“Na wewe hupendi?” Tausi akamwuliza.
“Sio hivyo rafiki yangu. Mimi nilikuwa napendezewa na hizo rangi zako nzuri na natamani na mimi ningeweza kuwa na rangi kama hizo. Si bora ungenipa na mimi hiyo siri yako ili na mimi niwe mzuri kama wewe?”
Tausi akacheka sana, “Ha ha ha Ha ha ha” mpaka akawa hawezi kujizuia. Kinyonga akashangazwa na hali hii ya tausi mwishowe akamuuliza akamuuliza, “ni kitu gani kimekuchekesha namna hiyo?”

Tausi kwa taabu akajizuia huko kucheka kwake na kumjibu, “Umenichekesha rafiki yangu kwa sababu vipi utapata uzuri kama wangu au siri gani hiyo nikupe uweze kujibadilisha? Kwani mimi sikujiumba mwenyewe kuwa hivi…”
Kinyonga akamkatiza maneno kwa kumwambia, “Sawa kama hutaki kunisaidia, wewe ringa tu, mimi nitatafuta njia mwenyewe.” Tausi akamtizama kwa mshangao akiwaza je huyu Kinyonga ataweza vipi kujigeuza?  Kinyonga akaondoka na huzuni na masikitiko akimwacha Tausi na fikra.

Mapambazuko ya siku ya pili na mapema yalimpata Kinyonga tayari yuko njiani kujitafutia njia ya kujigeuza na ndio akakutana na Kombomwiko.
“Habari ya asubuhi Mende.”
“Nzuri sana Kinyonga. Je mbona na asubuhi mapema leo? Unaelekea wapi?”
“Ah rafiki yangu pengine hata wewe utaweza kunisaidia.”
“Niambie rafiki yangu, nikiweza nitakusaidia,” akajibu Kombomwiko.
Basi Kinyonga akaendelea, “Mimi natamani sana niwe na rangi mwilini kama vile Tausi na sijui nifanye vipi hata niweze kupata rangi hizo. Je unaweza kunisaidia kimawazo?”
Kombomwiko akamjibu,“Ah! Kwani rangi yako ina nini? Si mimi pia niko na rangi moja mwili mzima na nimeridhika nayo? Hivi ndivyo tulivyoumbwa.”

Kinyonga akaona hapa hatopata msaada wowote akamwambia Kombomwiko, “Basi wewe bakia hivyo hivyo, mimi nitaendelea kutafuta njia ya kuweza kujigeuza rangi niwe kama Tausi. Kwaheri.” Akashika njia yake na kumwacha Kombomwiko na wazo kama za Tausi; je ni vipi ataweza Kinyonga kujigeuza rangi ya mwili wake?




Kinyonga akaendelea na safari yake na baada ya muda akakutana na paka akamtangulizia salamu.
“Paka hujambo?”
“Sijambo Kinyonga. Leo mbona uko mbali huku na makao yako ya kawaida?” Paka akauliza.
“Niko njiani nikitafuta namna ya kujigeuza niwe na rangi nzuri nzuri kama Tausi…”
Hata kabla hajamaliza matamshi yake, Paka akamkatiza na kicheko cha ajabu.
“HAHAHA HAHAHA HEHEHE….” Aliangua kicheko kile huku akiwa chali mara akijipindua hivi na vile maana aliona ajabu kuwa Kinyonga aliamini ataweza kujigeuza rangi ya mwili wake.

Kinyonga alipoona namna anavyocheka paka kwa stihizai alikasirika na kuondoka huku akilini akijiambia, “Nitamwonesha huyu Paka kuwa naweza kujigeuza!”.....

Je Kinyonga ataweza kubadilisha rangi ya mwili wake? Ungana na mimi wakati ujao Mungu akipenda tufatilie hadithi hii!