Mwandishi: Naima Baghozi
Unaweza kusoma sehemu ya 2: http://strokesofmypen.blogspot.co.ke/2016/12/kinyonga-na-tausi-sehemu-ya-pili.html
Maskini Kinyonga akajitizama na kuona michirizi ya rangi iliyokuwa ikitiririka kutoka mwilini mwake. Moyo ulimuuma na machozi kumbubujika buji buji akiuona urembo wake huooo unamtoka. Kombamwiko alimbembeleza sana na kujaribu kila njia ya kumnyamazisha lakini wapi…ndio mwanzo Kinyonga alikuwa anazidisha kilio mpaka mwisho Kombamwiko akamwambia: “Sikiza rafiki yangu, usilie sana. Naona ni bora urudi kwa Tumbiri umuombe akusaidie tena na sasa umeshajua ukiona mvua ukimbie wala usikaribie maji yoyote, sawa?”
Kinyonga hapo akapata moyo kidogo na kuamua kufanya hivyo. “Shukrani sana Kombamwiko kwa nasiha yako nzuri, naona ndivyo nitakavyofanya. Kwaheri kwa sasa , wacha nianze safari ya kwenda kwa Tumbiri , tutaonana.”
“Kwaheri ya kuonana na nakutakia kila la heri.”
Kinyonga akashika njia ya kurudia huko huko alikotoka. Safari yenyewe ilikuwa si fupi lakini aliamua kwenda hivyo hivyo maana lengo lake ni kubadili rangi ya mwili wake. Basi akaenda kwa mwendo wa kasi kadiri alivyoweza mpaka alipofika nusu ya njia akakutana na Sungura katika shughuli zake za kuchimba chimba akijitafutia chakula.
Akamsalimia kwa furaha : “Aah! Sungura rafiki yangu, habari za siku nyingi?” Sungura akamjibu : “ Nzuri Kinyonga. Ni kweli tumepotezana kwa muda mrefu sana. Hivi unaelekea wapi?”
“Kwa vile nimekuona wewe pengine sina haja ya kwenda nilikokuwa ninaenda.”
“kwani ulikuwa unaenda wapi? Na mimi ninaweza kukusaidia vipi?” Sungura akauliza tena.
“Wewe Sungura, sote tunakufahamu kwa ujanja na werevu wako ndio nimeona wewe utaweza kunipa ushauri bora nipate lengo langu.” Basi Kinyonga akaendelea na kumweleza kisa chake tangu mwanzo hadi mwisho.
Sungura akamuuliza: “Kwa ufupi unataka uwe na rangi kama za Tausi au sivyo?”
“Ndivyo,” akajibu Kinyonga.
Sungura akamwambia : “Mimi naona bora uende kwa Tausi umuombe akutolee manyoya mawili matatu hivi ujifutilie juu ya mwili wako na pengine utakuwa na rangi kama yeye.”
Kinyonga akashangaa sana na na huku akiwaza vipi tangu mwanzo hakufikiria hivyo. “Aah! Sungura si nimesema wewe u mwerevu sana, utakuja na mimi unisaidie kumwomba Tausi?”
Sungura akakubali kurudi naye. Walipotaka kuondoka walimuona Tumbiri anakuja. Alipowasili aliwasalimia na kuuliza kilichokuwa kinaendelea na sababu ya Kinyonga kutokuwa na rangi. Basi Kinyonga akamweleza kile kilichotokea na walichokuwa wananuia kufanya yeye na Sungura.
Tumbiri akamuonea huruma na kumwambia : “Usihuzunike rafiki yangu hata mimi nitakwenda na nyinyi tukamtaradhie kwa vizuri Tausi ili akupatie hayo manyoya yake.”
Basi safari ya watatu hao ikaanza kwa mwendo wa haraka. Mara njiani wakamkuta Paka, nae aliona mbio walizokuwa wanakuja nazo. Mwanzoni alikuwa hajamwona Kinyonga lakini walipomkaribia akamuona Kinyonga bila ya rangi rangi zake akaanza na kicheko chake: “Hahahaha, hehehehe Kinyonga hahaha ziwapi rangi zako?” Kinyonga kwa hasira akawaambia Tumbiri na Sungura: “Mwacheni huyu Paka na ujinga wake. Twendeni zetu.” Wakaondoka kwa haraka. Paka akaamua kuwafuata nyuma nyuma ajue wanakwenda wapi na wanakwenda kufanya nini.
Bila ya kujua kama Paka anawafuata kisirisiri, Kinyonga na maswahibu zake waliendelea na safari yao ya kwenda kwa Tausi. Kabla ya kuwasili kwa Tausi wakampata Kombamwiko mbele yao. Akamuuliza Kinyonga: “Mbona rafiki yangu umerudi hivyo hivyo bila kupaka rangi zako?”
Kinyonga akamweleza nini wameamua kufanya. Basi Kombamwiko akaamua kuwafuata. Msafara ukaendelea mpaka kwa Tausi. Tausi kama kawaida alikuwa akizunguka zunguka kwa maringo katika bustani. Mara akauona msafara unamwingilia wa Tumbiri, Sungura, Kinyonga na Kombamwiko.
Asiyemuona alikuwa ni Paka maana alikuwa amejificha wasimuone. Hamu yake nikutaka kujua kuna sababu gani ya wote hawa kuja mpaka kwa Tausi. Tausi mwenyewe aliona ajabu kuwaona wote hawa pamoja kwani kwa kawaida kila mmoja huwa kivyake. Akaona bora awaulize: “Habari zenu? Muna nini leo, mbona mmeandamana kuja kwangu?”
Akajibu Sungura: “Nzuri Tausi. Sisi tumejikusanya kwako na ombi dogo tukutaradhie kama utaweza kutusaidia. Tausi akashangaa huku akiwaza ombi gani hilo lililowafanya hawa wote kujikusanya na kuja kwake. Akaamua kutaka kujuwa: “Ombi gani hilo? Hebu niambieni na nikiweza nitakusaidieni."
Tumbiri akapata moyo kidogo akasongea mbele na kusema: "Tausi, wewe unajua vizuri vipi Kinyonga anatamani kuwa na mwili wa rangi rangi kama wewe sivyo?"
Tausi akajibu: "Naam ni kweli, kwa hivyo munataka mimi nifanye nini?"
Kinyonga akajisogeza mwenyewe na kumweleza mambo yote yaliyojiri tangu alipoachana na yeye mpaka muda ule walipofika kwake. Akamalizia na kusema:
"Sasa nakuomba unisaidie na manyoya yako mawili matatu ili nijipake mwilini mwangu na pengine nitakuwa na rangi nzuri kama zako."
Rafiki zake nao wakazidi kutilia mkazo ombi hilo: "Tafadhali Tausi, tafadhali sana, msaidie maskini amesumbuka sana..." wakaendelea hivyo kwa muda kumnasihi Tausi ili akubali. Wakati wote huo Paka alikuwa amejificha juu ya mti karibu kuanguka kwa kujizuia na kicheko maana kila akikaa anastaajabu kwa nini Kinyonga ana lazima ya kujibadilisha rangi yake.
Tausi naye alipoona Kinyonga ananyenyekea sana pamoja na rafiki zake moyo wake ukaingia imani na kuamua: "Sawa nimekubali kumpatia Kinyonga manyoya yangu...lakini sijui kama yatamsaidia..."
-------------------------------------------------------------------------------------------------------------
Itaendelea karibuni in shaa Allah :)